Na Thobias Mwanakatwe, SINGIDA
MAMLAKA ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imetoa wito kwa walimu na wadau wote wa elimu nchini kujizatiti zaidi kwenye umahiri wa somo la Hisabati na matumizi yake ikiwamo kutumia zana za kidijitali katika ufundishaji badala ya nadharia pekee.
Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Dk. Jabir Bakari, amesema hay oleo (Septemba 2, 2025) katika hotuba yake iliyosomwa kwa niaba yake na Meneja wa TCRA Kanda ya Kati-Dodoma, Mhandisi Asajile John wakati akifungua mafunzo endelevu ya walimu wa hisabati kutoka mikoa yote nchini na Mkutano Mkuu wa Chama cha Walimu wa Hisabai Tanzania.
“Natoa wito pia kwa walimu mliopo hapa, Chama cha Walimu wa Hisabati Tanzania (MAT/CHAHITA) na wadau wa elimu kuendelea kuongeza ubunifu wa ufundishaji wa somo la Hisabati, kwa kupunguza pengo kati ya taaluma na sekta na kukuza ubunifu na uvumbuzi wa wanafunzi na kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuboresha vipaumbele kwa somo la Hisabati nchini,”amesema.
Amesema MAT,CHAHITA kwa kushirikiana na shule na halmashauri nchini zianzishe na na kuimarisha Klabu za Hisabati na za kidigitali ngazi ya shule ili kuondokana na dhana potofu iliyojengeka kwa jamii kwamba somo hilo haliwezekaniki.
Dk.Bakari amesema TCRA inatambua umuhimu mkubwa wa somo la Hisabati ambalo jamii imejenga dhana potofu ya kuwa haliwezekani, lakini ni somo pia lenye changamoto nyingi katika ufundishaji na ujifunzaji katika ngazi zote za elimu.
“Kupitia MAT/CHAHITA walimu mna nafasi nzuri ya kuendelea kufuta dhana potofu juu ya somo la Hisabati kwa vitendo kwa kupeana uzoefu wenye lengo la kuboresha ufundishaji na ujifunzaji wa somo hili katika shule zetu pamoja na kubadilishana uzoefu katika mada zenye changamoto za ufundishaji na ujifunzaji,” amesema.
Ameongeza kuwa Klabu za Hisabati shuleni zitakapoanzishwa na kuimarisha zilizopo nchini kutasaidia kukuza vipaji vya Hisabati na kujenga uelewa sahihi wa umuhimu wa sayansi na teknolojia kwa wanafunzi na walimu pia.
Dk.Bakari amesema ujenzi wa Taifa imara na maendeleo endelevu hauwezi kufikiwa kama ufahamu wa somo la Hisabati utaendelea kuwa chini kwani maendeleo tunayoyahitaji kwenye maeneo yote ya uchumi yanahitaji sana umahiri wa Hisabati kwenye jamii yetu.
“Wajibu huu mkubwa kwa Taifa Letu, unaanza na wewe mwalimu wa hisabati, tukirejea makazini, tukafundishe watoto wetu kwa upendo na furaha ya moyoni ili waweze kulipenda somo letu na pia tufundishe kwa kutumia zana ikiwepo vifaa vya teknolojia,”amesema.
Amesema walimu wa Hisabati wana nafasi ya kuendelea kuainisha kwa wanafunzi matumizi ya Hisabati katika maisha ya kila siku, kwenye sayansi na teknolojia na kuyatumia vizuri wakati wa ujifunzaji ili kuleta mvuto na kujenga uelewa kwa wanafunzi ili waweze kuona matumizi halisi6 kwenye maisha ya kawaida.
“Hesabu zinazofundishwa kuanzia shule za awali mpaka elimu ya juu kama namba, Aljebra, Logic, Probability, Seti, kalkulasi, jiometri na statistics kwa uchache ni muhimu sana kwa kumtayarisha mwanafunzi kuingia kwenye ulimwengu wa kidijitali na teknolojia zinazoibuka (emerging technologies),” amesema.
“Tuna watoto wenye hazina ya akili nzuri, wanaohitaji tu kujengwa kwenye misingi ya kuwaingiza kuwa wabobevu wa Hisabati na muendelezo wake kwenye matumizi yake (application) na kutoa mchango mkubwa kwenye uchumi wao binafsi, jamii zao lakini kwa Taifa letu la Tanzania katika zama hizi za uchumi wa kidijiti,” amesema Dk.Bakari.
Amesema TCRA kama taasisi inayosimamia sekta ya mawasiliano hapa nchini, imechukuwa hatua mbalimbali za makusudi kuendelea kuhamasisha uelewa, uvumbuzi na uendelezaji wa vipaji vya wanafunzi kwa kuweka mazingira ya usimamizi yanayochagiza kuongeza uzalishaji na ukuaji wa miundombinu wezeshi ya kidijiti.
Aliongeza kua uwepo wa miundombinu ya kidijiti, intaneti ya kasi (ICT Infrastructure) inayowezesha uwepo wa matumizi ya huduma za kidijiti katika dunia ya sasa kwani kwa kila ongezeko la asilima 10 kwenye “Broadband” na matumizi yake inaweza kusababisha au kuleta ongezeko la asilimia 2.5 katika Pato la Taifa kwa nchi zinazoendelea.
Mkurugenzi huyo wa TCRA amesema ujenzi wa Taifa imara na maendeleo endelevu hauwezi kufikiwa kama ufahamu wa somo la Hisabati utaendelea kuwa chini kwani maendeleo tunayoyahitaji kwenye maeneo yote ya uchumi iwe uchukuzi, mawasiliano, ufundi, ujenzi, viwanda, fedha, madini, kilimo, maji, takwimu, sayansi na teknolojia yanahitaji sana umahiri wa Hisabati kwenye jamii yetu.
Amesema TCRA inatambua kwamba kuna juhudi kubwa za MAT/CHAHITA katika harakati za kuboresha elimu ya Hisabati nchini kupitia shughuli za kitaifa na kama vile, Siku ya Hisabati (International Day of Mathematics - IDM) au siku Pai na mitihani ya mashindano kwa wanafunzi (Tanzania Mathematics Olympiads TAMO (Junior and Senior)).
“Pia napongeza juhudi kubwa inayofanywa na Chama hiki cha kitaaluma kwa kupanua wigo wa kushirikiana na Chuo kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) hasa idara ya Hisabati kwa kusaidia kuendeleza shughuli za chama ikiwemo ufadhili wa kufanyika mitihani ya TAMO. Natoa wito kwa Vyuo Vikuu vingine viige ili kusaidiana na Serikali katika kupunguza changamoto za somo la Hisabati, Mwenyezi Mungu awabarikiwe sana,”.
Naye Mwenyekiti wa Chama cha Hisabati Tanzania (MAT/CHAHITA), Dk.Said Sima, amesema baadhi ya mafanikio yaiyopatikana tangu kuanzishwa kwa chama hicho ni kupata ushindi wa mashindano ya Afrika (PAMO) 2024 na 2025 nchini Afrika Kusini na Botswana kwa kupata medali nne za saba kila mwaka.
Mafanikio mengine ni kuogeza hamasa na motisha kwa walimu wa Hisabati hata katika changamoto za uhaba wa walimu na miundombinu,kuelimisha na kukumbusha juu ya matumizi ya hisabati katika maisha na kujifunza juu ya akili mnemba faida na changamoto zake.
Dk.Sima amesema pamoja na mafanikio hayo lakini pia kumekuwa na changamoto ya ufaulu hafifu wa somo la hisabati,ukosefu wa fedha za kuendeshea kazi mbalimbali za chama katika kutekeleza malengo yake na mahudhurio hafifu ya walimu katika mafunzo yanayosimamiwa na chama.
MWISHO











Post a Comment