Na Jumbe Ismailly MANYONI
MAKAMPUNI manne ya Mkoani Tabora yanayonunua tumbaku katika wilaya ya Manyoni,Mkoani Singida yanadaiwa na vyama vya ushirika vya msingi vinne vya Halmashauri ya Itigi jumla ya dola za kimarekani 1,491,450.62 walizochukua tumbaku ya msimu wa kilimo uliopita.
Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha ushirika Mkoa wa tumbaku Manyoni (CEAMCU),Athumani Ibrahimu Swedi alisema kiasi hicho cha dola za kimarekani kinachodaiwa na vyama vya ushirika vya msingi kinatokana na zaidi ya kilo za tumbaku 1,242,875 zilizochukuliwa na makampuni hayo ya tumbaku.
Aidha Swedi aliyataja makampuni yanayodaiwa na vyama hivyo kuwa ni pamoja na Magefa dola 1,034,615.67,Biexen dola 408,853.89, Farmours rocic dola 43,132.09 na Mirambo Leaf dola 4,848.97.
Mwenyekiti huyo hata hivyo alivitaja vyama vya ushirika vya msingi vinavyodai kiasi hicho cha fedha na kampuni inayodaiwa ikiwa kwenye mabano kuwa ni pamoja na Isingiwe,Umoja na Luhanga(Magefa), Mwamagembe,Tumaini,Kalangali na Chikola (Biexen),Mitundu (Farmours rocic) na Mgandu (Milambo Leaf).
Kwa mujibu wa Swedi licha ya jitihada za uongozi wa chama kikuu hicho kwenda makao makuu ya kampuni hayo Mkoani Tabora kufuatilia madai hayo, makampuni hayo yaliahidi kwamba hadi ifikapo septemba,10,mwaka huu yangekuwa yamelipa madeni yote ya wakulima hao,ahadi ambayo mpaka sasa haijatekelezeka.
Mwenyekiti huyo hata hivyo aliweka bayana kuwa Mkuu wa wilaya ya Manayoni,Daktari Vincenti Mashinji amechukua hatua za kuyaita ofisini kwake makampuni yote sept,29,mwaka huu ili kujua sababu za kutotekelezwa kwa ahadi hiyo iliyotolewa na makamapuni hayo.
Swedi hata hivyo alitumia fursa hiyo kutoa wito kwa wakulima wa vyama vya ushirika kuanza kujiandaa na kilimo cha msimu ujao wa kilimo kwa kufuata taratibu na kanuni bora za kilimo cha tumbaku.
MWISHO.

Post a Comment