Na Comrade Japhari Saidi
Baada ya kifo cha ghafla cha Hayati Rais John Pombe Magufuli mnamo mwaka 2021, zilisikika tetesi kuwa baadhi ya watu hawakutaka aliyekuwa Makamu wa Rais, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, kuapishwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kama ambavyo Katiba ya nchi yetu inavyoelekeza.
Awali tulidhani hizo ni tetesi za mitaani zisizo na uzito. Lakini baadaye, kupitia mahojiano ya aliyekuwa Mkuu wa Majeshi, tulithibitishiwa kwamba kweli kulikuwapo na mpango wa kuzuia hatua hiyo ya kikatiba.
Kwa bahati nzuri, vyombo vyetu vya ulinzi na usalama vilisimama imara na kuhakikisha Katiba inaheshimiwa. Makamu wa Rais aliapishwa kuwa Rais halali wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na akaendelea kuhudumu kwa kipindi kilichobaki.
Tukiwa tunaelekea uchaguzi wa mwaka 2025, Rais Samia Suluhu Hassan ni kiongozi aliyehudumu kwa kipindi cha miaka minne na miezi kadhaa kinachohesabika kama awamu moja kwa mujibu wa katiba.
Kwa mujibu wa mila, desturi na utamaduni wa CCM, Rais aliyeko madarakani huachwa amalizie kipindi chake cha pili bila kupingwa, kama ilivyotokea kwa marais wastaafu: Mwinyi, Mkapa, Kikwete, na Magufuli.
Hata hivyo, kwa mshangao, limeibuka kundi la watu, akiwemo Bwana Humphrey Polepole, wakidai kuwa Samia hakupaswa kupitishwa kuwa mgombea. Wanadai kuwa Makamu wa Rais, Waziri Mkuu au Spika huwa hawateuliwi kugombea Urais kupitia CCM.
Japo wana CCM tunakumbuka vizuri tuu kwamba Waziri Mkuu Mstaafu Salim Ahmed Salim aliteuliwa na Kamati Kuu ya CCM kuwania Urais mwaka 2005 na akaenda hadi tatu bora aliposhindwa na Jakaya Kikwete. Ndio kusema kama kura zake zingetosha ndiye angekuwa mgombea Urais wa CCM mwaka 2005.
Hata kama ni kweli hakujawahi kutokea mgombea Urais wa CCM kuwa aliyekuwa Makamu wa Rais, Waziri Mkuu au Spika,
Swali muhimu ni hili: Je, Samia Suluhu Hassan aliyepitishwa kuwa mgombea Urais ni Makamu wa Rais, Spika au Waziri Mkuu? Bila shaka jibu ni hapana. Yeye ni Rais aliyeko madarakani kwa awamu yake ya kwanza. Hivyo hoja ya Polepole haina mashiko na inapingana na misingi ya historia ya CCM.
Kama ndugu Polepole atakubali kuwa Samia ni Rais halali aliye kwenye muhula wake wa kwanza, basi ni lazima pia akubali kuwa mila, desturi na utaratibu wa CCM vinatuelekeza kumpitisha kumalizia kipindi chake cha pili bila kupingwa — kama ilivyokuwa kwa watangulizi wake wote tangu mfumo wa vyama vingi uanze.
Ni wakati sasa wa kulinda umoja wa chama, kuheshimu utamaduni wa chama na kuacha siasa za mizengwe, fitina na chuki.
Mwisho.


Post a Comment