Na Mwandishi Wetu
Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Singida (SIREFA), Hamisi Kitila, ameongoza hafla ya fainali ya Ligi ya Wilaya ya Singida Daraja la Nne, ambapo ametumia nafasi hiyo kutoa pongezi na maelekezo muhimu kwa wadau wote wa soka katika wilaya hiyo.
Akiwa kama mgeni rasmi, Kitila aliwapongeza Chama cha Mpira wa Miguu Wilaya ya Singida (SIDIFA) kwa kuandaa na kusimamia mashindano hayo kwa uadilifu na kufuata kanuni na taratibu kama inavyotakiwa. Alisisitiza umuhimu wa kuacha mazoea na kuwataka viongozi wa vilabu kufuata miongozo ya kisasa katika uendeshaji wa timu.
“Mpira wa sasa unahitaji uwazi, maandalizi ya kitaalamu na matumizi ya mifumo ya kisasa. Hili linawezekana endapo viongozi wetu watajifunza, kushirikiana na kuwa na nidhamu ya kazi,” alisema Kitila.
Aidha, alisisitiza umuhimu wa kuwa na data bezi ya wachezaji, akisema hatua hiyo itaongeza ufanisi katika ufuatiliaji wa vipaji na kusaidia maendeleo ya mpira katika ngazi ya mkoa na taifa.
Katika fainali hiyo, Kitila alifurahishwa na uwepo wa wachezaji wapya waliovutia wadau wa soka, akimpongeza Katibu wa SIDIFA kwa kazi nzuri ya kuratibu ligi kwa kufuata miongozo na kanuni za mchezo.
Kwa upande wa Singida Manispaa, ligi hiyo ya daraja la nne ilishirikisha timu 9, zilizogawanywa katika makundi 2, ambapo jumla ya mechi 20 zilichezwa hadi bingwa kupatikana. Viwanja vilivyotumika ni Gereza la Singida, Mwenge Secondary, na Airtel Ground.
Mwenyekiti Kitila aliwapongeza Mungu Maji FC kwa kutwaa ubingwa wa ligi hiyo kwa msimu huu, na kuwahimiza kuendelea kujenga nidhamu, maadili na maandalizi ya kimashindano wanapojiandaa kupanda daraja na kushiriki ligi ya juu zaidi.
Mwisho, alihimiza kuendelea kuandaa mashindano ya mpira wa miguu mara kwa mara ili kutoa fursa kwa wachezaji, vilabu na wadau mbalimbali kuendeleza mchezo wa soka mkoani Singida na taifa kwa ujumla.
Credit: Abdul Bandola


Post a Comment