Na Thobias Mwanakatwe
JOTO la kisiasa katika majimbo yaliyopo mkoani Songwe limeamza kupanda baada ya Mbunge wa Tunduma, David Silinde kudaiwa kuandaa vijana kumzuia mbunge wa Momba, Condester Sichalwe asihudhurie mkutano wa Baraza la Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Wilaya ya Momba.
Tukio la kuzuiliwa Condester lilitokea Jumamosi (Aprili 19, 2025) wakati wa mkutano wa Baraza la UVCCM uliofanyika katika Shule ya Sekondari Tunduma na kuhudhuriwa na viongozi wa CCM na UVCCM wa Wilaya ya Momba.
Silinde ambaye pia ni Naibu Waziri wa Kilimo alipopigiwa simu mara kadhaa ilikuwa inaita tu bila kupokelewa lakini alipotumiwa ujumbe mfupi wa maneno (sms) hakukataa wala kukubali kama alihusika kupanga vijana wa kumzuia mbunge Sichalwe kuingia kwenye kikao badala yake alimtaka mwandishi kuwasiliana na Mwenyeki wa Katibu wa UVCCM Wilaya ya Momba.
"Mpigie mwenyekiti au katibu wa vijana wa Wilaya ya Momba nadhani ndio watu sahihi kukupa majibu ya maswali yako maana mengine ndio nasikia kwako," alisema Silinde baada ya kuandikiwa sms na mwandishi kwamba anadaiwa kuhusika kuandaa vijana kumzuia mbunge wa Momba asiingie kwenye kikao hicho.
Katibu wa UVCCM Wilaya Momba, Thomas Warioba, alipoulizwa kuhusu tukio hilo alisema ni kweli vijana wa 'green guard' walimzuia mbunge Sichalwe asiingie, hata hivyo hakueleza sababu za vijana hao ambao wanatoka jimbo la Tunduma kufanya kitendo hicho.
"Waliomzuia mbunge Sichalwe asiingie kwenye kikao cha UVCCM Wilaya walikuwa vijana wa green guard na sio kweli kwamba waliandaliwa na mbunge wa Tunduma Silinde wale ni vijana wa hamasa wa UVCCM," alisema ingawa hakuweka wazi nani aliyewatuma kufanya tukio hilo.
Naye Mwenyekiti wa UVCCM Wilaya ya Momba, Mandela Mtaki, alipoulizwa kuhusu tukio hilo alikiri kutokea lakini akasema hawezi kulizungumzia kwa undani kwasababu limeshafikishwa kwa Katibu wa CCM Wilaya ya Momba ambaye ndiye anayeshughulika nalo.
"Suala hili mimi siwezi kulizungumzia lilivyotokea nakuomba muulize Katibu wa CCM wa Wilaya yeye ndiye ana mamlaka ya kuzungumzia suala hilo na sio sisi viongozi wa UVCCM," alisema.
Katibu wa CCM Wilaya ya Momba,Kataba Sukulu, alipoulizwa kwa njia ya simu alisema baada ya tukio kutokea alitoa maelekezo na kukemea kitendo alichofanyiwa mbunge Sichalwe.
"Tamko gani tena la chama unataka nitoe wewe sikiliza ile 'clip' hadi mwisho utasikia maelezo niliyoyatoa baada ya tukio hilo kutokea," alisema katibu huyo na kukata simu.
Mbunge wa Momba,Condester Sichalwe, alipoulizwa alisema ni kweli alizuiliwa kuingia kwenye mkutano wa UVCCM Wilaya ambao mgeni rasmi alikuwa Mbunge wa Tunduma, David Silinde licha ya kwamba na yeye alialikwa.
Alisema vituko vilianza kwa kuzuia gari lake kwa kupanga magari ili asiweze kupita baada kutoka kwenye kikao cha Mfuko wa Jimbo lakini baadaye alimua kushuka kwenye gari lake na kuanza kwenda ukumbini.
Sichalwe alisema baada ya kufika karibu na lango la kuingilia ukumbini vijana wa green guard walimzuia na alipohoji alielezwa kuwa wamepewa maelekezo na viongozi kwamba yeye (Sichalwe) asiingie kwenye mkutano huo.
Taarifa za ndani kutoka katika kikao hicho zinaeleza kuwa mbunge huyo baada ya kuzuiliwa Katibu wa CCM wa Wilaya alipewa taarifa na kuingilia kati ambapo alikemea kitendo kilichofanywa na vijana wa green guard na Sichalwe aliingia ukumbini na kuendelea na kikao.
Mbunge Sichalwe licha ya kupata msukosuko wa kuzuwiliwa, baada ya kupewa nafasi ya kuzungumza kwenye mkutano huo alitekeleza ahadi yake ya kutoa Sh.milioni moja kwa ajili ya kusaidia UVCCM lakini katika hali ya kushangaza Mwenyekiti wa UVCCM alikataa kuipokea.
Taarifa za ndani zinaeleza kuwa kuna msuguano mkali ambapo inadaiwa Silinde katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu anataka kuondoka jimbo la Tunduma na kwenda kugombea jimbo la Momba ambalo mbunge wake wa sasa ni Condester Sichalwe hivyo anatumia kila mbinu kumdhoofisha Sichalwe.
MWISHO


Post a Comment