Na Mwandishi Wetu, Dodoma
Kwa mara ya pili, Mamlaka
ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imeshinda tena tuzo ya
Uhusiano Mwema na Vyombo vya habari nchini, kwa mwaka 2024 ikidhihirisha namna
taasisi hiyo inavyothamini ushirikano na uhuru wa vyombo vya habari katika
kuuhabarisha umma kuhusu shughuli za udhibiti wa huduma za nishati na maji.
Tuzo hiyo iliyotolewa
jana(29.3.2024) na Chama cha Maofisa Uhusiano Tanzania (PRST), baada ya mchuano
mkali uliohusisha taasisi nyingi imeipa EWURA heshima na ari ya kuendelea
kudumisha uhusiano wake thabiti na vyombo vya habari pamoja na waandishi wa
habari nchini.
Meneja Mawasiliano na
Uhusiano wa EWURA, Bw. Titus Kaguo alisema ushindi huo kwa mara ya pili
mfululizo ni kielelezo cha utawala bora, uwazi, uwajibikaji, na miongozo
inayotolewa na Bodi na Menejimenti ya EWURA, chini ya mwemyekiti wake Prof.
Mark Mwandosya na Mkurugenzi wake Mkuu, Dkt. James Mwainyekule.
Vigezo vilivyotumika
kuipatia EWURA ushindi huo ni kuwa na mpango mkakati bora wa ushirikishwaji wa
vyombo vya habari, ubora wa maudhui na uthabiti wa utoaji taarifa pamoja na
mtazamo walionao vyombo vya habari kuhusu Mamlaka hiyo.
Wakati huo huo, Bi.
Janeth Mesomampya, ambaye ni Ofisa Uhusiano wa EWURA amepokea tuzo ya Ofisa
Uhusiano bora kwa mwaka 2024, akiwa mmoja wa washindi watano katika tuzo hizo.
Rais wa PRST Bw. Assah
Mwambene, alisema utoaji wa tuzo hizo ni chachu kwa wataalam walioko kwenye
kada hiyo kufanya kazi zao kwa ubora zaidi ili kuimarisha huduma katika maeneo
yao ya utendaji.
EWURA ilipata tuzo ya
aina hiyo pia kwa mwaka 2022, iliyotolewa na PRST kutambua mchango wake katika
kushirikiana vyema na vyombo vya habari nchini.


Post a Comment