Na Mwandishi Wetu
Watu saba wamepoteza maisha na wengine 17 kujeruhiwa katika ajali ya barabarani iliyohusisha lori na basi dogo aina ya Coaster yenye namba ya usajili DVD 370 katika eneo la Mlima Sekenke, wilayani Iramba mkoani Singida.
Ajali hiyo ilitokea majira ya saa 4:00 asubuhi wakati lori lililokuwa likishuka mlima huo likidaiwa kupata hitilafu ya mfumo wa breki na kuligonga kwa nyuma basi hilo lililokuwa likitoka Singida kuelekea Igunga mkoani Tabora.
Kwa mujibu wa taarifa za awali kutoka eneo la tukio, baada ya kugongana, magari yote mawili yalitumbukia kwenye korongo lililopo kando ya Barabara Kuu ya Dar es Salaam–Mwanza na kusababisha vifo na majeruhi hao.
Mashuhuda wa tukio hilo wamesema kuwa lori hilo lilionekana kushindwa kudhibiti mwendo wake kabla ya kuligonga basi hilo, hali iliyosababisha ajali hiyo kubwa.
Naye Mganga Mkuu wa halmashauri ya Wilaya ya Iramba Dkt. Peter Luhega Janga, amesema majeruhi 17 waliopatikana katika ajali hiyo wamepokelewa hospitali ya Wilaya ya Iramba kwa ajili ya kupatiwa matibabu ambapo miongoni mwao mmoja alifariki hospitalini. Amesema. Juhudi za kutoa msaada na kuwatambua marehemu zikiendelea kufanywa na vyombo vya usalama pamoja na wananchi.
"Tumepokea miili ya watu sita (6) ambao walifariki katika eneo la ajali, wanaume wanne na wawili wakiwa watoto wakike na majeruhi 17 ambapo mmoja alifariki hospitalini" Dkt. Peter Janga.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Singida, Halima Dendego, alifika katika eneo la ajali hiyo na baadaye hospitalini ambapo ametoa pole kwa familia zilizopoteza wapendwa wao na kuwatakia nafuu ya haraka majeruhi wote wanaoendelea kupatiwa matibabu.
Amesema serikali inaendelea kufuatilia kwa karibu hali ya majeruhi pamoja na kuchunguza chanzo halisi cha ajali hiyo ili kubaini mazingira yote yaliyosababisha kutokea kwake.
Aidha, amewataka madereva kuzingatia sheria za usalama barabarani na kuhakikisha magari yao yanakuwa katika hali nzuri ya kiufundi kabla ya kuanza safari, hususan katika maeneo yenye miteremko mikali kama Mlima Sekenke.
Uchunguzi wa tukio hilo unaendelea kufanywa na Jeshi la Polisi Wilaya ya Iramba mkoani Singida.





Post a Comment