Na Mwandishi Wetu
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imetangaza kuanza kwa mchakato mpana wa mapitio ya kanuni, sheria na ada za leseni zinazosimamia vyombo vya habari vya mtandaoni nchini, hatua inayolenga kujibu malalamiko ya muda mrefu ya wadau wa sekta ya habari.
Akizungumza katika kikao kazi kilichowakutanisha viongozi wa Serikali, mabloga na waandishi wa habari mtandaoni, Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Dkt. Jabiri Kuwe Bakari, alisema Serikali imeamua “kusikia kilio” cha wadau waliodai kuwa mfumo wa sasa unakandamiza ubunifu na kuua ajira kwa vijana.
Dkt. Bakari alisema gharama kubwa za leseni na urasimu wa kikanuni vimekuwa vikwazo vikubwa vinavyowafanya waandishi wengi kushindwa kurasimisha shughuli zao. Ili kupata suluhu ya kudumu, amewaelekeza wadau kupitia TBN na JUMIKITA kuteua wajumbe wanne watakaoungana na jopo la wataalamu wa TCRA kuandaa mapendekezo ya mabadiliko ya ada na sheria.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Tanzania Bloggers Network (TBN), Beda Msimbe, aliwasilisha uchambuzi unaoonyesha kuwa Tanzania ina vizingiti vikubwa ikilinganishwa na nchi nyingine za Afrika Mashariki. Alieleza kuwa mwanablogu wa Tanzania analazimika kulipa kati ya shilingi 500,000 hadi 1,000,000, huku Kenya kukiwa hakuna hitaji la leseni ya gharama hiyo na Uganda ada ikiwa kati ya shilingi 60,000 hadi 100,000.
Alisisitiza kuwa hali hiyo inawalazimisha mabloga kutumia mtaji wao kulipia ada za Serikali badala ya kuwekeza katika vifaa bora kama kamera na maikrofoni, jambo linalopunguza ushindani wa kimataifa.
Akizungumza katika kikao hicho, Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, alisema Serikali ya Awamu ya Sita imejipanga kuachana na mfumo wa adhabu kwa wanahabari wa mtandaoni na badala yake kuanza mkakati wa uwezeshaji wa kiuchumi.
Msigwa alitangaza kuwa Serikali inapanga kuanzisha mfuko maalum wa kuwawezesha mabloga na waandishi wa mtandaoni kumiliki vitendea kazi vya kisasa na kukuza taaluma zao. Alisema maelekezo ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha mabloga, wengi wao wakiwa Gen Z, wanatambuliwa kama washirika muhimu wa maendeleo.
Aidha, Msigwa aliahidi Serikali kukutana na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ili kutatua changamoto za kodi zinazowakabili mabloga, akisisitiza kuwa blogu zitambuliwe kama biashara ndogo (SMEs) badala ya kuzitazama kama vyombo vikubwa vya habari.

.jpeg=w378-h243-p-k-no-nu)
Post a Comment