VIJANA WAHIMIZWA KULINDA AMANI YA TAIFA LA TANZANIA

 

Na Mwandishi Wetu, Singida



Afisa Maendeleo ya Vijana Mkoa wa Singida, Ndugu Frederick Ndahani, amewahimiza vijana wa mkoa huo kuendeleza na kulinda amani iliyopo nchini Tanzania. Ndahani alitoa wito huo wakati akizungumza na vijana wa Chama cha Skauti na kufungua Kundi la Skauti katika Shule ya Sekondari Manguanjuki iliyopo katika Manispaa ya Singida.



Akizungumza katika hafla hiyo, Ndahani alisema kuwa baadhi ya vijana nchini wameanza kuiga mitindo na mienendo isiyo mizuri kutoka mataifa mengine, jambo ambalo linaweza kuhatarisha amani iliyojengwa kwa zaidi ya Miaka 64.



“Kila mtu ana uraia wake, na sisi vijana wa Tanzania uraia wetu ni wa Kitanzania. Tunapaswa kuendelea kuilinda amani ya Nchi yetu kwa manufaa yetu na vizazi vijavyo,” alisema Ndahani.



Aidha, aliwahimiza vijana wa Skauti kutimiza ahadi zao kwa Mungu na Taifa kwa kuwa wazalendo, watiifu, na walinzi wa amani na mali za umma. Alisisitiza kuwa ni jukumu la kila kijana kutoa taarifa kwa vyombo vya ulinzi na usalama pindi wanapoona dalili za uvunjwaji wa amani au uharibifu wa mali za umma.



“Ni muhimu kwa kila kijana kulinda mali za umma na hata mali za wawekezaji. Wengi wao wamewekeza nchini na kuwaajiri vijana wengi. Tukiharibu amani, tunapunguza uwekezaji na kuathiri utalii ambao ni chanzo cha mapato ya fedha za kigeni,” aliongeza Ndahani.



Kwa upande wake, Kamishina wa Skauti Wilaya ya Singida, Bi. Veronica Mwambuta, aliwataka wanachama wa Skauti kutojihusisha na vitendo vya vurugu au uvunjwaji wa amani vinavyofanywa na baadhi ya vijana nchini.



Naye Enetha Mathias, mwanaskauti kutoka Shule ya Sekondari Manguanjuki, alisema wako tayari kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama katika kufichua watu wenye nia ya kuharibu amani. Pia aliitaka Serikali kuendelea kushirikiana na makundi yote ya kijamii, ikiwemo wazee, vijana, viongozi wa dini na vyama vya siasa, ili kudumisha maridhiano na kuendeleza amani ya nchi.

                                             MWISHO

Post a Comment

Previous Post Next Post