MAKINDA AFUNDA WANAWAKE KUHUSU UCHAGUZI MKUU 2025

 

Na Thobias Mwanakatwe,SINGIDA 



SPIKA mstaafu wa Bunge, Anne Makinda, amewataka wanawake kuondokana na dhana  potofu kwamba hata wasipoenda kupiga kura siku ya Uchaguzi Mkuu Rais Dk.Samia Suluhu Hassan atapita tu kwani suala la uchaguzi sio la mchezo.


Alisema hayo jana wakati akizungumza na mamia ya wanawake wa Mkoa wa Singida katika kongamano la wanawake wa mkoa huo lililoandaliwa kwa ajili kumpongeza Rais Samia kutokana na maendeleo makubwa aliyoyafanya katika Mkoa wa Singida.



"Uchaguzi hakuna mchezo kila mtu awajibike kisheria aende asubuhi mapema kupiga kura usiseme mama atapita tu hakuna cha kusema atapita tu," alisema Makinda.


Makinda alisema kila inapofika wakati wa uchaguzi kumekuwa na tabia kwa baadhi ya watu kwamba hata wasipoenda kupiga kura viongozi wanaowataka watapita tu jambo ambalo sio rahisi hivyo.


"Yaani unasema hata nisipopiga kura atapita tu na wanaosemaga hayo ni sisi wanawake tunasema Samia ameshapita sio hivyo nendeni kapigeni kura," alisema.


Alisema wanawake na wananchi kwa ujumla watambue kuwa hata katika imani za dini usipoenda kupiga kura kwa ajili ya kumchagua viongozi ni dhambi.


Makinda alisema wanawake lazima wamuunge mkono Rais Samia kwani ameleta mageuzi makubwa ya maendeleo nchini na hivi sasa amekuwa kinara wa matumizi ya nishati safi na kuachana na matumizi ya nishati chafu ambayo imekuwa ikileta madhala kiafya kwa wanawake.



Aidha,Makinda amewataka wanawake  kutunza vizuri kadi za kupigia kura kwani kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu huwa vinaibiwa au baadhi ya watu wanavinunua kutokana na maslahi yao binafsi.


"Nchi hii ndugu zangu mjiweke vizuri hivyo vichinjio (kadi za kupigia kura) vinaibiwa wanaweza kuibiwa hivi hivi kwenye mfuko wako au wanaweza kununua wanakuja na pesa wananunua, vilindeni mviweke mahali pazuri," alisema Makinda.



Naye Mkuu wa Mkoa wa Singida, Halima Dendego, alisema katika uchaguzi wa serikali za mitaa uliofanyika mwaka jana wanawake 900 wa mkoa wa huu walichukua fomu kugombea ueneyejikiti wa vijiji,vitongoji na ujumbe wa serikali za vijiji  ambapo kati yao 109 wamefanikiwa kuchaguliwa kuwa viongozi.


Alisema katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu wa wanawake ambao wamejipima wajitokeze kugombea nafasi ya ubunge na udiwani kushindana na wanaume kwani nafasi hizo ni za wote na sio kwamba zipo kwa ajili ya wanaume tu.



Dendego alisema Rais Dk.Samia Suluhu Hassan ameleta maendeleo makubwa katika Mkoa wa Singida ambapo suala la umeme vijiji 441, vitongoji 1052 vimefikishiwa huduma ya umeme na vitongoji 120 kazi ya kupeleka umeme inaendelea.


"Mkoa wetu umepokea majiko gesi ya ruzuku 30,111 ambayo yatauzwa kwa bei ya Sh.20,800 badala ya Sh.48,000 na tutahakikisha wananchi wote wanaanza kutumiza nishati safi," alisema Dendego.


Alisema katika sekta ya afya ndani ya kipindi cha utawala wa Rais Samia zimejengwa zahanati mpya 62,vituo vya afya 22 na hospitali mpya za wilaya zimejengwa nne.


Mkuu wa Mkoa alisema katika sekta ya elimu Shule mpya za msingi 12,sekondari 40 na shule za amali 7 zimejengwa na upatikanaji wa maji umefikia asilimia 86 kutoka asilimia 53 iliyokuwepo awali na miradi 39 inatekelezwa na hadi Disemba itakuwa imekamilika.


MWISHO

Post a Comment

Previous Post Next Post